Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- mawasiliano hayo ya simu, ambayo yalithibitishwa na vyanzo tofauti kwa gazeti New York Times na vyombo vya habari kama El País na France 24, yalifanyika siku chache kabla ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuiweka “Karti ya Jua (Cartel de los Soles)” inayohusishwa na Maduro na makamanda wake, katika orodha ya mashirika ya kigaidi. Kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na mazungumzo hayo, mawasiliano yalikuwa “sahihi na yenye heshima,” na Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, pia alihudhuria mazungumzo hayo. Pia kulikuwa na majadiliano kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mkutano nchini Marekani, ingawa hadi sasa hakuna mpango wa mwisho uliowekwa.
Mawasiliano haya ya moja kwa moja yanakinzana na misimamo mikali ya Trump, ambaye siku ya Alhamisi alitangaza kuwa operesheni ya ardhini dhidi ya wauzaji dawa za kulevya wa Venezuela “itafanyika hivi karibuni.” Haya yanajiri ilhali mashambulizi ya awali ya majini katika Karibi na Bahari ya Pasifiki yamesababisha vifo zaidi ya 80, na Marekani haijatoa uthibitisho wowote kwamba walengwa wa mashambulizi hayo walihusishwa na biashara ya dawa za kulevya. Umoja wa Mataifa umetaja kuwa mashambulizi hayo huenda yakachukuliwa kama mauaji ya kiholela nje ya utaratibu wa kisheria, na Venezuela inasisitiza kuwa lengo halisi ni kumuondoa Maduro madarakani kwa kisingizio cha kupambana na dawa za kulevya.
Upelekaji wa majeshi ya Marekani katika eneo hilo unajumuisha maelfu ya wanajeshi, makumi ya ndege za kijeshi, meli ya kubeba ndege za kivita USS Gerald R. Ford, pamoja na rada mpya nchini Trinidad na Tobago — hatua ambayo Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Kamla Persad-Bissessar, ameithibitisha kuwa ni kwa madhumuni ya “kuboresha ufuatiliaji dhidi ya wasafirishaji haramu.” Kwa upande wa Venezuela, Jeshi limewekwa tayari; Maduro ameiagiza Jeshi la Anga kuwa katika tahadhari na, katika maandamano makubwa, amesisitiza juu ya umoja wa kitaifa akisema: “Katika kipindi hiki nyeti kwa uhai wa Jamhuri, hatuna budi kushinda.”
Mgogoro wa anga pia umeongeza mvutano, ambapo serikali ya Venezuela imefutia vibali mashirika ya ndege kama Iberia, TAP, Avianca, LATAM, Turkish Airlines na GOL kutokana na kusimamisha safari zao, na ikasema kuwa hatua hizo zinahusiana na kile ilichokiita “ugaidi wa kiserikali” wa Marekani. Trump, kwa upande wake, ameunganisha vitisho na ishara za kibalozi akisema kuwa “mazungumzo ili kuokoa maisha” yanaweza kuwa chaguo, ingawa alitoa onyo kwa Maduro kuhusu kuwaruhusu wahamiaji haramu na wanachama wa magenge kama Tren de Aragua kuingia Marekani.
Wachambuzi wanasema mawasiliano haya ya simu yanaweza kuwa hatua ya mwanzo kuelekea kujenga daraja la kidiplomasia, lakini kutokana na mkakati wa mvutano na upunguzaji wa mvutano unaofanywa kwa zamu na Ikulu ya White House, hali ya kutokuwa na uhakika bado inaendelea kutawala.
Your Comment